Joshua 9

Udanganyifu Wa Wagibeoni

1 aBasi ikawa wafalme wote waliokuwa magharibi mwa Yordani waliposikia juu ya haya yote, wale waliokuwa katika nchi ya vilima, upande wa magharibi mwa vilima na katika pwani yote ya hiyo Bahari Kuu,
Yaani Bahari ya Mediterania.
hadi kufikia Lebanoni (wafalme wa Wahiti, Waamori, Wakanaani, Waperizi, Wahivi na Wayebusi),
2 c dwakajiunga pamoja ili kupigana vita dhidi ya Yoshua na Israeli.

3 eHata hivyo, watu wa Gibeoni waliposikia juu ya hayo yote Yoshua aliyowatendea watu wa Yeriko na Ai, 4nao wakaamua kufanya hila: Wakajifanya kama wajumbe wakiwa na punda waliobebeshwa mizigo wakiwa na magunia yaliyochakaa na viriba vya mvinyo vikuukuu vyenye nyufa zilizozibwa. 5Walivaa miguuni mwao viatu vilivyoraruka na kushonwa kisha wakavaa nguo kuukuu. Chakula chao kilikuwa mkate uliokauka na kuingia koga. 6 fNdipo wakamwendea Yoshua kambini huko Gilgali wakamwambia yeye pamoja na watu wa Israeli, “Tumetoka katika nchi ya mbali, fanyeni mkataba nasi.”

7 gBasi watu wa Israeli wakawaambia hao Wahivi, “Lakini huenda mnakaa karibu nasi, twawezaje basi kufanya mapatano nanyi?”

8 hWakamwambia Yoshua, “Sisi ni watumishi wako.”

Yoshua akawauliza, “Ninyi ni nani, nanyi mnatoka wapi?”

9 iNao wakamjibu: “Watumishi wako wametoka nchi ya mbali sana kwa ajili ya umaarufu wa Bwana Mwenyezi Mungu wenu. Kwa kuwa tumesikia taarifa zake: hayo yote aliyofanya huko Misri, 10 jpia yale yote aliyowatendea wafalme wawili wa Waamori mashariki ya Yordani; huyo Sihoni mfalme wa Heshboni na Ogu mfalme wa Bashani, aliyetawala huko Ashtarothi. 11Basi wazee wetu na wale wote wanaoishi katika nchi yetu walituambia, ‘Chukueni chakula cha safari; nendeni mkakutane na watu hao na kuwaambia, “Sisi tu watumishi wenu, fanyeni mapatano nasi.” ’ 12Mkate huu wetu ulikuwa wa moto tulipoufunga siku tulipoanza safari kuja kwenu, lakini sasa angalia jinsi ulivyokauka na kuota ukungu. 13Viriba hivi vya mvinyo vilikuwa vipya tulipovijaza, lakini ona jinsi vilivyo na nyufa. Nguo zetu na viatu vimechakaa kwa ajili ya safari ndefu.”

14 kBasi watu wa Israeli wakavikagua vyakula vyao bila kupata shauri kutoka kwa Bwana. 15 lNdipo Yoshua akafanya mapatano ya amani pamoja nao kuwaacha waishi, nao viongozi wa kusanyiko wakathibitisha kwa kiapo.

16Siku ya tatu baada ya hao kufanya mapatano na Wagibeoni, Waisraeli wakapata habari kuwa hao watu ni jirani zao waliokuwa wanaishi karibu nao. 17 mNdipo wana wa Israeli wakasafiri na siku ya tatu wakafika kwenye miji yao ya Gibeoni, Kefira, Beerothi na Kiriath-Yearimu. 18 nLakini Waisraeli hawakuwashambulia kwa kuwa viongozi wa kusanyiko walikuwa wamewaapia kwa Bwana, Mungu wa Israeli.

Kusanyiko lote likanung’unika dhidi ya hao viongozi,
19lakini viongozi wote wakawajibu, “Tumeshawaapia kwa Bwana, Mungu wa Israeli, kwa hiyo hatuwezi kuwagusa sasa. 20 oHivi ndivyo tutakavyowafanyia: Tutawaacha waishi, ili ghadhabu isije juu yetu kwa kuvunja kiapo tulichowaapia.” 21 pWakaendelea kusema, “Waacheni waishi, lakini wawe wapasua kuni na wachota maji kwa ajili ya jamii yote.” Hivyo ahadi waliyoweka viongozi kwao ikawa hivyo.

22Kisha Yoshua akawaita Wagibeoni na kuwaambia, “Kwa nini mmetudanganya kwa kutuambia, ‘Tunaishi mbali nanyi,’ wakati ambapo ninyi mnaishi karibu nasi? 23 qSasa mko chini ya laana: Daima mtakuwa wapasua kuni na wachota maji kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu.”

24Wakamjibu Yoshua, “Watumwa wako waliambiwa waziwazi jinsi Bwana Mwenyezi Mungu wenu alivyomwamuru mtumishi wake Musa kuwapa ninyi nchi hii yote na kuwaangamiza wakazi wake wote toka mbele zenu. Kwa hiyo tuliogopa mno kwa ajili ya uhai wetu kwa sababu yenu, ndiyo maana tukafanya neno hili. 25 rSasa tupo mikononi mwako. Tufanyieni lolote mnaloona kuwa jema na haki kwako.”

26Kwa hiyo Yoshua akawaokoa mikononi mwa Waisraeli, nao hawakuuawa. 27 sSiku hiyo Yoshua akawafanya Wagibeoni wapasua kuni na wachota maji kwa ajili ya jamii na kwa ajili ya madhabahu ya Bwana mahali pale ambapo Bwana angepachagua. Hivyo ndivyo walivyo hadi hivi leo.
Copyright information for SwhKC